Serikali imesema hadi kufikia Agosti mwaka huu, deni la Taifa lilifikia Trilioni 52.303 kulinganishwa na Tsh. Trilioni 49.283 katika kipindi cha Agosti, mwaka jana ambapo kiwango hicho ni sawa na ongezeko la Tsh. Trilioni 3 katika kipindi cha mwaka mmoja.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango alibainisha kuwa kati ya deni hilo, Deni la Ndani lilikuwa Trilioni 14.075 na Deni la Nje Trilioni 38.227 na kusema kuwa ongezeko la deni lilichangiwa na kupokewa kwa mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2018, ilionesha Deni la Serikali bado ni himilivu katika muda mfupi, wa kati na mrefu kwa viwango vya kimataifa na Serikali inaendelea kuhakikisha deni linakuwa himilivu kwa kuhakikisha mikopo inayokopwa inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo yenye tija kwa Taifa.
Kuhusu mwenendo wa viashiria vya uchumi, Dkt. Mpango amesema Uchumi wa Taifa umeendelea kuwa imara ambapo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita (2009 – 2018), Pato halisi la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.4 kwa mwaka.