Baada ya Mahakama Kuu kusitisha kusikiliza rufaa ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, leo December 6 wamerudishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kesi yao ya msingi.
Mbowe na Matiko walikata rufaa baada ya Mahakama ya Kisutu kuwafutia masharti dhamana, November 23,2018.
Katika kesi ya msingi, Mbowe, Matiko na Viongozi wengine saba wa CHADEMA wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na uchochezi.
Wakili wa utetezi Peter Kibatala amemwambia Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa washtakiwa wote wapo isipokuwa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Kawe Halima Mdee.
Mdhamini wa Mdee alisimama na kuieleza mahakama kuwa, aliwasiliana na Mdee amemwambia anaenda nchini Burundi kushiriki michezo ya Kibunge na atarudi December 20,2018.
Wakili wa serikali, Faraja Nchimbi amesema anakiri kupokea taarifa ya Mdee na Heche ambaye bado anamuuguza mke wake, hivyo hana pingamizi.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mashauri amewataka washtakiwa wasiokuwepo mahakamani wafike December 20, ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi December 21,2018.
Mbali na Mbowe, Msigwa na Matiko, washtakiwa wengine ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.
BAADA YA SIKU 14 GEREZANI, MBOWE, MATIKO WARUDISHWA MAHAKAMANI, BONYEZA PLAY HAPA CHINI KUTAZAMA