Mitandao ya kijamii imejitokeza na kuendelea kuwa vyombo vya kusambaza habari na taarifa mbalimbali na kwa mifumo mbalimbali. Ili kupata habari na taarifa zilizo sahihi, watumiaji wa mitandao ya jamii wanapaswa kujilinda dhidi ya habari na taarifa za uongo na uzushi.
Watumiaji wanaotegemea mitandao kama vyanzo vya habari au taarifa wanaweza kutambua iwapo
habari na taarifa hizi ni za uongo, uchochezi,uzushi au za kutusi watu wengine. Kuna namna za kugundua iwapo habari ni ya ukweli au la.
1. Kuwa na mashaka na vichwa vya habari vyenye mbwembwe: Habari nyingi za uongo zinakuwa na
vichwa vya habari vilivyoandikwa kwa maneno na mpangilio unaoonyesha mbwembwe. Iwapo utaona kichwa cha habari chenye maneno ambayo kwa harakaharaka unashuku ukweli wake, kuna uwezekano mkubwa kwamba habari hiyo sio ya kuaminika.
2. Angalia vizuri anwani ya tovuti inayotumika: Kila tovuti ina anwani inayotambulika kimataifa na inaanza na herufi ‘www’. Angalia kwa makini anwani ya tovuti yenye habari. Iwapo habari iko kwenye anwani ya uongo au ambayo imeghushiwa ni dhahiri kwamba ni ya uongo.
Mitandao mingi yenye habari za uongo inatumia anwani ambazo kwa haraka unaweza kudhania kwamba ni za mitandao ya habari inayoaminika. Ukiona hili, tembelea anwani ya uhakika na linganisha na ya mtandao wenye habari unayoishuku.