Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa Wizara, Mikoa na Wilaya kuhakikisha kero na malalamiko wananchi wanyonge yanatafutiwa ufumbuzi haraka badala ya kuwaacha wakipigwa danadana.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo wakati akizungumza na wananchi akiwa njiani kutoka Mugumu kwenda Tarime katika eneo la daraja la mto Mara Wilayani Serengeti na Nyamongo, Nyamwaga na Tarime Mjini Wilayani Tarime ambako ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Mara.
Kabla ya kutoa maagizo hayo Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la mto Mara lililopo katika barabara inayounganisha Mugumu na Tarime ambalo lina urefu wa meta 94, upana meta 9.9, ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 75 na litagharimu shilingi Bilioni 8.5 hadi kukamilika.
Akizungumza na wananchi baada ya kukagua ujenzi wa daraja hilo Rais Magufuli amesikiliza kilio cha Mama mmoja mwenye upofu aitwaye Nyambura Nyamarasa aliyedai mazao yake yameliwa na mifugo, na kwamba juhudi za kufuatilia haki yake hazijafanikiwa huku akiendelea kuhangaika.
Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu ambaye hajachukua hatua licha ya Mama huyo kumpelekea kilio chake, na ameagiza vyombo vya dola vimkamate mtu anayedaiwa kulisha mifugo katika shamba la Mama huyo na kumfikisha katika vyombo vya sheria.
“Viongozi niliowachagua na mnaofanya kazi na Serikali ninayoongoza, nataka kuona mnashughulikia matatizo ya watu wanyonge, sitaki kuona watu wenye fedha wanawanyanyasa masikini, na kweli leo nilitaka kukufukuza kazi Mkuu wa Wilaya, nakusamehe lakini kashughulikie haki ya huyo Mama na viongozi wote hakikisheni watu wanyonge hawanyanyaswi”.
“Rais akina Mama wanatembea usiku na hawabakwi” Waziri Kangi Lugola