Inatokea baadhi ya mikoa kuonekana kama ina idadi kubwa ya wagonjwa wa akili kuliko mikoa mingine wapo wanaohusisha wagonjwa hao wa akili na imani za kishirikina pengine bila kujua chanzo kinachopelekea maradhi hayo kutokea.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Magonjwa ya akili Dr.Frank Aloyce Masao kutoka Muhimbili March 27 2014 ametoa taarifa na chanzo cha magonjwa ya akili ambapo anaanza kwa kusema>>’Kimsingi sababu zinazosababisha magonjwa ya akili zimegawanywa katika makundi makuu 3′
‘Kuna kundi la kwanza ambalo ni kundi la kimwili sisi kitaalam tunaita Biological reasons ambazo zinatokana na mtu mwenyewe kwa mfano sehemu kubwa ya wagonjwa wa akili wana vina saba vinavyosababisha maradhi ya akili, ugonjwa wa akili ni ugonjwa wa kurithi toka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine’
‘Ili ugonjwa wa akili uweze kutokea yapo mambo mengine yanayosababisha ila kuna baadhi ya mambo tu yanaweza kuchangia mfano akiugua ugonjwa kama Malaria, unakuta kimsingi mtu anakua mgonjwa hivyo anapougua malaria au uti wa mgongo au maradhi mengine kama kifafa yanaweza kusababisha ugonjwa wa akili’
‘Matumizi ya pombe ni miongoni mwa sababu zinazoweza kuchochea ugonjwa wa akili ukaonekana kwa hivyo matumizi ya pombe,matumizi ya bangi n.k. ni vizuri tukatambua matumizi ya vilevi hasa bangi sio sababu hasa ya msingi ya kumfanya mtu akaugua ugonjwa wa akili’
‘Kimsingi mgonjwa wa akili anakua na vina saba vya ugonjwa wa akili ila matumizi ya vilevi kama bangi na pombe vinaweza kuchangia kufanya huo ugonjwa kuonekana, hii imekua ni sababu mojawapo inayochangia unyanyapaa katika jamii’
‘Tathmini zetu zinaonyesha kati ya asilimia 3-5 ya wanaovuta bangi wanaweza kupata maradhi ya akili wakati asilimia zilizobakia ambao wanavuta bangi huwa hawapati maradhi ya akili, hii haimaanishi kwamba naiambia jamii ivute bangi ila naiasa kujua si kila anayeugua ugonjwa wa akili anatumia bangi’
‘Kundi la pili ni kundi la Saikolojia yapo matatizo mbalimbali ya kisaikolojia yanayoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa mfano mtu aliyebakwa, mtu aliyefikwa na majanga, mtu aliyepata ajali siku za nyuma, mikwaruzano katika ndoa, ugumu wa maisha na mahangaiko mbalimbali yanaweza kuchangia mtu kupata maradhi ya akili’
‘Kundi la tatu ni la kijamii ambalo sababu za kijamii na za kisaikolojia huwa zinaenda pamoja kwa maana zinahusiana zaidi na mambo ya kimahusiano, kundi hili pia linaweza kusababisha mtu akapata maradhi ya kiakili’.