Timu ya madaktari kutoka Marekani imethibitisha kuwa mlinda mlango wa Liverpool, Loris Karius alipoteza fahamu baada ya kugongwa kichwani na kiwiko cha Sergio Ramos katika mchezo wa fainali ya UEFA Champions League.
Mlinda mlango huyo alifanyiwa vipimo katika hospitali ya Massachusetts jijini Boston na timu ya wataalamu waliomfanyia vipimo wanaamini kuwa makosa aliyoyafanya Karius katika mchezo huo yalitokana na upotevu huo wa fahamu.
Kwa mujibu wa madaktari hao Karius anaendelea vema na wanategemea atapona vizuri kabisa.
Ikumbukwe kuwa baada tu ya Karius kugongana na Ramos alifanya makosa mawili yaliyopelekea timu yake kuadhibiwa na Real Madrid 3-1 katika fainali ya UEFA.
Karius ameachwa katika kikosi cha timu yake ya taifa ya Ujerumani kitakachoshiriki kombe la dunia nchini Russia.