Mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani Tanga zimezidi kuleta maafa, baada ya usiku wa kuamkia leo Oktoba 26, 2019 kukata barabara kati ya Handeni na Korogwe katikati ya kijiji cha Misima na Sindeni.
Pichani ni gari la abiria aina ya Noah likiwa limetumbukia mtoni, Noah hiyo inayodaiwa ni ya abiria na ilikuwa inatoka Handeni kwenda Korogwe, ilipofika hapo alfajiri ya leo, dereva hakujua kuwa barabara imekatika, hivyo akajikuta anaingia kwenye mto. Inadaiwa watu kadhaa wamepoteza maisha.
Pia taarifa zingine zinaripotiwa kuwa Abiria zaidi ya 5,000 waliokuwa wanasafiri kutoka DSM na Mikoa ya jirani wamekwama toka jana katika eneo la Mandela kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya barabara katikati ya wilaya ya Handeni na Korogwe, Tanga baada ya mto Mandera kufurika maji.
DC Korogwe Kissa ameandika katika ukurasa wake Instargram “Tumekutwa na mvua zisizo za kiasi. Tunaendelea Kumuomba Mungu kutunusuru. Aidha Serikali inaendelea kuchukua hatua ya kuzuia maafa zaidi hasa kutokea kwa watu.”
“Ndio mana magari yamezuiliwa kutokupita maeneo hatarishi. Lipo eneo la Daraja la Mandela, zuio njia ya Korogwe – Handeni daraja la Sindeni limekatika na njia ya Korogwe- Muheza kupitia mnyuzi mto Luhengera umejaa.” DC Kissa
“Haya ni maafa yanaletwa na Mungu mwemyewe hakuna anayeweza kuzuia kikubwa tuwe watulivu na wavumilivu huku tukichukua tahadhari. Zaidi ya yote wananchi maeneo tulioambiwa tuhame kama tahadhari nawasihi mfanye hivyo ni jitahda ya kuokoa maisha ya watu waliopo maeneo hatarishi.” DC Kissa
“Poleni sana wanakorogwe, poleni watanzania wenzangu mliokwama Korogwe. Hali ya sasa maji yanapungua mandela ila bado hakupitiki. Shukrani kwa Jeshi la polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Tanroads na Tarura kwa jitahda zao katika maafa haya. Kazi kubwa inayoendelea ni kuhakikisha watu na mali zao wapo salama.” DC Korogwe