Sudan imemteua Waziri Mkuu mpya ikiwa nchi hiyo ipo kwenye utawala wa mpito wa miaka mitatu chini ya Uongozi wa Jeshi.
Waziri Mkuu Abdalla Hamdok anasema kuwa kipaumbele chake ni upatikanaji wa amani na kutatua changamoto za kiuchumi.
Uteuzi wake umekuja wakati ambapo Luteni Abdel Fattah Abdelrahman Burhan alichaguliwa kuwa kiongozi mpya wa baraza huru.
Serikali mpya itaongoza taifa hilo mpaka kipindi cha uchaguzi. Kumekuwa na vurugu kwa miezi kadhaa ambayo imesababisha vifo vya waandamanaji wengi.
Upande wa upinzani una matumaini kuwa uteuzi mpya utaweza kusaidia kumaliza utawala wa kijeshi.
Hamdok ameapishwa kama Waziri Mkuu wa mpito alipowasili kutoka Ethiopia, eneo alilokuwa akifanyia kazi kama Mtaalamu wa Uchumi wa Umoja wa Mataifa (UN) tangu mwaka 2011 kabla ya kuacha kazi hiyo mwaka jana.
“Vipaumbele vya kwanza vya Serikali ni kusitisha vita, kuimarisha usalama, kukuza uchumi na kujenga uhusiano mzuri na sera za mataifa ya kigeni,” alisema Hamdok
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Mwaka jana, Hamdok alichaguliwa na Bashir kushika nafasi ya Waziri wa Fedha lakini alikataa.