Leo October 14, 2018 Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kuhakikisha fikra na mipango mizuri aliyoiweka inatekelezwa kwa manufaa ya Watanzania wote.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani Jijini DSM alikokwenda kumtembelea muda mfupi baada ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu ya Jumapili iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay.
Rais Magufuli amebainisha kuwa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere alifanya kazi kubwa ya kujenga misingi imara ya nchi kuwa na amani, umoja na mshikamano na pia kujenga misingi ya uchumi wa kujitegemea kupitia Azimio la Arusha.
Ametoa wito kwa Watanzania wote hasa vijana kuungana na Serikali katika kuyaenzi yaliyofanywa na Baba wa Taifa, na pia kuliombea Taifa.
Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amemshukuru Rais Magufuli kwa kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa na amemhakikishia kuwa yeye na wanamaombi wenzake pamoja na Watanzania wote wanamuombea heri yeye, viongozi wote na Taifa kwa ujumla.
Aidha, akiwa nyumbani hapo Rais Magufuli aliyeongoza na Mkewe Mama Janeth Magufuli amekutana na mtoto wa Baba wa Taifa Makongoro Nyerere na Wajukuu wa Baba wa Taifa.
Mapema leo asubuhi Rais Magufuli ameungana na Waumini wa Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay Jijini Dar es Salaam kusali Misa Takatifu ambapo Waumini hao wamemuombea Baba wa Taifa, aliyefariki dunia tarehe 14 Oktoba, 1999.
Millard Ayo, Shetta na Hanscana msibani kwa Pancho Gairo