Leo August 30, 2018 Wizara ya Afya, imetuma Mtaalamu Bingwa wa uchunguzi (Pathologist) kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando mkoani Mwanza kwa ajili ya kuchunguza upya mwili wa mtoto Sperius Eradius ambaye amefariki dunia siku chache zilizopita kufuatia adhabu ya kupigwa shuleni.
Waziri wa Afya Ummy Mwalim kupitia akaunti yake rasmi ya mtandao wa Twitter amesema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mtoto huyo na kuongeza kuwa tayari mtaalamu huyo ameshawasili mkoani Kagera kwa ajili kufanya uchunguzi huo.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mtoto Sperius Eradius aliyekuwa darasa la 5 S/Msingi Kibeta, Bukoba ambapo kimehusishwa na adhabu ya kupigwa na Walimu wake. Ninatoa pole kwa wazazi/walezi, ndugu na marafiki wa marehemu.Mungu awape moyo wa ustahimilivu”-Waziri Ummy
“Kufuatia wazazi wa mtoto kutokuwa na imani na uchunguzi uliofanywa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kagera, Wizara yangu imetuma mtaalamu bingwa wa uchunguzi (Pathologist) toka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya kwenda kufanya upya uchunguzi wa mwili wa marehemu” ameandika Waziri Ummy
“Tayari mtaalamu huyo ameshawasili Kagera leo asubuhi kwa ajili ya kuanza uchunguzi mpya. Ninatoa wito kwa familia, ndugu na wananchi kuwa watulivu ktk kipindi hiki ambapo uchunguzi wa kibingwa unaendelea. Tutahakikisha kuwa uchunguzi unafanyika kwa ufanisi ili haki itendeke” Waziri Ummy akitoa taarifa ya Daktai kufika
“Aidha nitumie fursa hii kuwataka Wazazi/Walezi na Walimu kutambua wajibu mkubwa tulionao wa kuwafundisha na kuwalea watoto wetu kwa kuzingatia sheria na taratibu tulizojiwekea. Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto havikubaliki katika jamii yetu na ni kinyume cha sheria za nchi” -Waziri Ummy
“Kama jamii tunao wajibu wa kuhakikisha mtoto anaishi, kukua na kuendelezwa ktk mazingira salama na rafiki kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya 2009. NINALAANI VIKALI Vitendo vya Ukatili vinavyofanywa dhidi ya watoto ktk jamii. Tutawafuatilia na kuwachukulia hatua wanaohusika” -Waziri Ummy
Awali uchunguzi wa mwili wa marehemu ulifanywa na Hospitali ya Rufaa ya mkoani humo, lakini wazazi wa marehemu wamesema kuwa hawana imani na uchunguzi huo na hivyo kuiomba serikali iweze kufanya utaratibu mwingine wa uchunguzi zaidi.