Miongo miwili iliyopita, siku moja baada ya Krismasi, tsunami ilipiga visiwa vya Koh Phi Phi, katika mkoa wa Krabi, kusini mwa Thailand. Katika nchi hii ya kifalme ambayo ilirekodi vifo zaidi ya 5,000, maumivu bado ni makubwa kwa wakaazi, ambao walinusurika na kupoteza wapendwa wao.
Nchini Thailand, ambako nusu ya watu zaidi ya 5,000 waliokufa walikuwa watalii wa kigeni, maombolezo yasiyo rasmi yalitarajiwa kufuatia hafla ya ukumbusho ya serikali.
Kumbukumbu kwenye fukwe na ibada za kidini zitafanyika kote Asia, hususan Indonesia, Sri Lanka, India na Thailand, ambazo ndizo zilizoathirika zaidi.
Mnamo Desemba 26, 2004, tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 9.1 karibu na ncha ya magharibi ya Indonesia lilisababisha mawimbi makubwa yaliyopiga pwani za nchi 14 kuanzia Indonesia hadi Somalia.
Indonesia ilipoteza watu zaidi ya 160,000, ikiwa ndiyo iliyoathirika zaidi. Katika mkoa wake wa magharibi wa Aceh, waombolezaji walikusanyika kwa dakika ya ukimya, kisha kutembelea kaburi la pamoja na kufanya sala ya kijumuiya katika msikiti mkuu wa mji mkuu wa mkoa huo, Banda Aceh.