Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji linasema kuwa zaidi ya Waethiopia milioni nne sasa wamekimbia makazi yao ndani ya nchi, hasa kwa sababu ya migogoro au ukame.
Ripoti ya Kitaifa ya Kuhama Makazi, ambayo inaangazia kipindi cha kati ya Novemba mwaka jana na Juni 2023, inasema theluthi mbili kati yao walilazimishwa kutoka makwao kutokana na migogoro.
Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2021 ripoti hiyo inajumuisha eneo lililokumbwa na vita la Tigray, ambalo lina wakazi wengi zaidi wa Ethiopia waliong’olewa na vita – zaidi ya watu milioni moja.
Eneo la Somalia mashariki mwa Ethiopia linashikilia idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na ukame.
Hapo awali Umoja wa Mataifa ulisema zaidi ya Waethiopia milioni 20 walikuwa wakihitaji msaada wa chakula na $4bn (£3.14bn) zilihitajika kukidhi mahitaji yao.