Fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ambayo itafanyika mwishoni mwa wiki hii siku ya Jumamosi, kati ya FC Barcelona dhidi ya Juventus, itakuwa ni tukio la aina yake kwa mtoto mmoja wa kitaliano aishiye Jiji la Milan.
Kijana huyo ana umri 14, kwa bahati mbaya alipata ajali ya kukwama kwenye maji yenye kina kirefu kwa zaidi ya dakika 40, akapoteza fahamu kwa muda wa wiki mbili.
Gazeti la The Independent linaripoti kwamba mtoto huyo ambaye jina lake ni Michael, alipata ajali hiyo baada ya yeye na rafiki zake watano kutoka kwenye daraja la mto mmoja katika Jiji la Milan, mwisho wake baada ya kuzama mapigo yake ya moyo yalisimama kwa muda huo, baada ya vipimo ilionesha alipata tatizo zaidi kwenye ubongo.
Wiki nne baada ya kulazwa hospitali alizinduka na jambo la kwanza kuuliza ilikuwa kuhusu timu yake anayoishabikia kama bado ipo kwenye michuano ya mabingwa wa ulaya.
Daktari ambaye alikuwa anamsimamia, Alberto Zangrillo daktari binafsi wa mmiliki wa AC Milan, Silvio Berlusconi alisema kupona kwa mtoto huyo ni jambo kubwa zaidi lililowahi kumtokea katika maisha yake ya udaktari kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo.
Mtoto Michael, Jumamosi hii tarehe 6 atakuwa miongoni mwa mashabiki wa Juventus watakaokuwa wakiombea ushindi timu yao itakapokuwa ikipambana na FC Barcelona, Jiji la Berlin, Ujerumani.