Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa @innocentbash ameungana na Wananchi na Wafanyabiashara wa Kata ya Bugene Wilayani Karagwe Mkoani Kagera katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Zahanati mpya eneo la Kishao katika Kata ya Bugene.
Bashungwa ameongoza harambee hiyo leo July 03 2023 iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Karagwe na Ofisi ya Mbunge kwa kushirikia na Diwani wa Kata ya Bugene, Mugisha Mathias, wakati akiongoza harambee hiyo, Bashungwa amechangia kiasi cha shilingi milioni 12 ambapo ameungwa mkono na Wananchi na Wafanyabiashara wa Bugene kwa kuchangia jumla ya Tsh. milioni 37,635,000 na saruji mifuko 26.
Bashungwa ametoa wito kwa Wananchi wa Jimbo la Karagwe kuunga Juhudi za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kujitoa kuchangia miradi ya maendeleo kama ilivyo kwa Wananchi wa Kata ya Bugene.
Aidha, Bashungwa ametumia nafasi hiyo kuwashukuru Wananchi wa Kata hiyo kwa kuchangia shilingi milioni 80.4 zilizotumika katika ujenzi wa Shule ya Sekondari mpya ya Omurushaka ambapo Serikali ilitoa milioni 580 kuunga mkono Juhudi za Wananchi ili kukamilisha Shule hiyo ambayo tayari imeshapokea Wanafunzi.