Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) zimeeleza kutiwa wasiwasi na tangazo la jeshi la Niger kuwa litamfungulia mashtaka rais aliyeondolewa madarakani, Mohamed Bazoum kwa tuhuma za kufanya uhaini mkubwa.
Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema tangazo hilo la jeshi la Niger linatia wasiwasi mkubwa.
Amesema, “Tungali tuna wasiwasi mkubwa juu ya hali, afya na usalama wa Rais (Bazoum) na familia yake; na kwa mara nyingine tunatoa mwito wa kuachiwa kwake mara moja, na kurejeshwa madarakani.”
Jumapili usiku, jeshi la Niger lilisema Bazoum na watu wa karibu yake watafunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kufanya uhaini mkubwa na kudhoofisha usalama wa ndani na nje.
Serikali ya mpito ya Niger imesema kuwa imekusanya ushahidi wa kumfungulia mashtaka rais huyo aliyeondolewa madarakani na washirika wake wa ndani na nje, kwa uhaini mkubwa na kuhatarisha usalama wa ndani na nje wa Niger.
Wakati huohuo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika imesema imeshtushwa na mpango huo wa wanajeshi wa Niger wa kumpandisha kizimbani rais Bazoum.
Taarifa ya ECOWAS imesema: Hatua hiyo ( ya kumshtaki Bazoum) ni aina fulani ya uchochezi wa mambo unaofanywa na viongozi wa mapinduzi, kinyume na kauli zao kuwa wana azma ya kufumbua mgogoro uliopo kwa njia ya amani.