Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza siku 4 za maombolezo kuanzia leo tarehe 21 Septemba, 2018 kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere katika ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 131 waliothibitika mpaka sasa.
Kivuko hicho kilipinduka na kisha kuzama majini jana mchana meta chache kabla ya kufika katika kisiwa cha Ukara kikitokea kisiwa cha Bugolora ambapo mpaka sasa watu 40 wameokolewa wakiwa hai, miili 131 imeopolewa na zoezi la uokoaji linaendelea.
Pamoja na kutangaza siku 4 za maombolezo Rais Magufuli amewapa pole wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hiyo, amewaombea majeruhi wapone haraka na amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Mwanza, vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi wote wanaoendelea kushiriki katika uokoaji.
“Kwa masikitiko makubwa nawapa pole wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hii, huu ni msiba mkubwa uliolikumba Taifa letu, nawaomba Watanzania wote kwa wakati huu ambapo vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea na uokoaji tuwe watulivu na tuendelee na kushikamana kama ilivyo desturi yetu, huu sio wakati wa kulumbana na kukatishana tamaa” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwapuuza wanaotaka kutumia ajali hii kujipatia umaarufu wa kisiasa, na amebainisha kuwa ni vema Watanzania wote tuungane kuwaombea Marehemu wapumzike mahali pema, majeruhi wapone haraka na kuwatia moyo wote wanaoendelea na zoezi la uokoaji.
Rais Magufuli amemtuma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwenda eneo la tukio, ameagiza kuundwa tume ya uchunguzi wa chanzo cha ajali hii na ameagiza wote waliohusika kusababisha ajali hii wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Taarifa za awali zimeonesha dhahiri kuwa kivuko cha MV Nyerere kilikuwa na idadi kubwa ya watu na mizigo kupita uwezo wake, kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi wa chanzo chochote cha ajali hii, tunatarajia kuwa ataupeleka mahakamani” amesisitiza Rais Magufuli.
HUZUNI: Miili inaelea, maiti 125 zimetolewa majini, Helicopter ziko hewani