Kuanzia May 1 2021 kumekuwepo na mjadala baada ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kuanza kutumia sheria ya kuzikagua nyimbo zote mpya za Wasanii kabla ya kupelekwa kwenye Radio au TV Nchini Tanzania ambapo utaratibu huo mpya unamlazimu Msanii kusubiri BASATA ipitishe wimbo wake na akabidhiwe cheti kisha wimbo upelekwa Redioni.
Wasanii wengi kwa asilimia kubwa pamoja na Wadau wa burudani wameonesha kutopendezwa na sheria hiyo na kutaka BASATA iachane na huo utaratibu au itafute utaratibu mwingine wa kudhibiti nyimbo zisizo na maadili lakini sio huu, sasa baada ya yote hayo Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Dr. Hassan Abbasi amejitokeza na kuongea yafuatayo.
“Nimefikishiwa maoni mengi na Wadau mbalimbali kuhusu agizo la Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kuhakiki kazi za muziki kabla hazijatoka na inaonekana BASATA wanaona ni njia ya kuboresha kazi na kulinda maadili”
“Wadau nao wana hoja kwamba huko ni kuleta urasimu usio na lazima, tutalimaliza hilo hivi ———> siku ya Jumamosi May 8 2021 Waziri wetu Innocent Bashungwa na mimi tutakaa kuwasikiliza BASATA na Wawakilishi wa Wasanii hoja kwa hoja kisha tutatoa uamuzi wa papo kwa hapo, hili limeisha👏🏽” —Dr. Hassan Abbasi