Leo July 2, 2018 Rais John Magufuli amewaapisha rasmi viongozi mbalimbali aliowateua jana baada ya kufanya mabadiliko mafupi.
Walioapishwa ni Kangi Lugola anayekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Mwigulu Nchemba.
Wengine ni Prof. Makame Mbarawa aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Maji na umwagiliaji, Eng. Isack Kamwele aliyeteuliwa kuwa Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Thomas Mihayo anayekuwa Kamishna wa Tume ya Uchaguzi(NEC), pamoja na makamishna wengine.
Ninakusogezea MAMBO5 yaliyosababisha Rais Magufuli kufanya mabadiliko Wizara ya Mambo ya Ndani.
Jambo la kwanza ni Ajali za Barabarani “Ajali za barabarani nimechoka kutuma rambirambi, unatuma hujakaa hata wiki unatuma tena, kinachosikitisha Waziri hatumi hata rambirambi wala haendi kuzika, unasikia tu yuko huko..! Hakuna hatua zinazochukuliwa”
Jambo la Pili ni ndani ya Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa “Kuna suala la NIDA, mambo ni hovyo kuna pesa zilichezewa, kuna vifaa viliagizwa na havikufika, tumewachukulia hatua lakini waliofanya mambo hayo mpaka leo hatua gani wamechukuliwa? Je, pesa hizo zimerudishwa? Kasimamie hayo mambo”
Jambo la Tatu ni uhaba wa Magari katika Jeshi la Zimamoto “Jeshi la Zimamoto kuna magari 53, mengine ya mwaka 1987, wahusika wenye wizara waliopewa wapo tu wala hawataki kuyajua haya, lakini kwenye sherehe wanahudhuria, ukasimamie haya, Zimamoto wawe na uwezo wa kupambana na haya majanga”
Jambo la Nne ni Waziri kutokutoa Rambirambi zinapotokea ajali na kutokwenda kuzika “Nimechoka kutuma salamu za rambirambi za ajali kila siku huku Waziri wa Mambo ya Ndani akiwa kimya wala haendi kuzika anazurura tu, Watu wanakufa kila siku; mnasubiri mpaka wafe wangapi ndipo mchukue hatua?”
Jambo la Tano ni “Mkoa wa Mbeya katika wiki mbili wamekufa watu 40, majeruhi zaidi ya 100, hakuna hatua zinazochukuliwa hata ya kuwambia RPC na RTO wajiuzulu. Au hadi wafe wangapi? mpunguzie hata nyota ili ajue damu za watu zinavyouma. Kaanze na RPC Mbeya”
RAIS MAGUFULI ‘NIMECHOKA KUTUMA RAMBIRAMBI’