Leo July 12, 2018 Wahasibu 3 wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wa kuisababishia shirika hilo hasara ya Shilingi Milioni 57.73 kwa kuiba vocha za simu.
Wahasibu hao ni Mercy Semwenda (49), Flora Bwahawa (54) na Hawa Tabuyanjaa (54).
Akiwasomea makosa yao mbele ya Hakimu Mkazi Augustine Rwizila, Wakili wa serikali mwandamizi Patrick Mwita amedai washtakiwa hao wana mashtaka 2.
Katika shtaka la wizi linamkabili Semwenda ambapo anadaiwa ametenda kosa hilo kati ya January 1 na September 2017 DSM.
Anadaiwa aliiba vocha za muda wa maongezi za Shilingi Milioni 44.3, pesa za mauzo ya vocha za Milioni 5.9 na fedha taslimu Shilingi Milioni 8.5 vyote vikiwa mali ya shirika hilo.
Katika kosa la kusababisha hasara linawakabili washtakiwa wote ambapo wanadaiwa wametenda kati ya January mosi na September 2017 katika ofisi za TTCL Dar es Salaam.
Wanadaiwa wameisababishia shirika hilo hasara ya Shilingi Milioni 57.7 kutokana na wizi huo.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa kuwa kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi, hivyo haina dhamana hadi Mahakama Kuu.
Wakili Mwita amedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika anaomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine, ambapo Hakimu Rwezile ameiahirisha hadi July 24,2018.