Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Abdoulaye Bathily, aliitangaza jana Jumanne kujiuzulu wadhifa huo ambao ameshikilia tangu Septemba 2022, akimrithi Mslovakia Jan Kubis, ambaye pia alijiuzulu mwaka 2021, baada ya diplomasia kudorora katika kutatua mzozo wa muda mrefu nchini Libya.
Bathily alimehusisha kujiuzulu kwake kama mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya na “kukatishwa tamaa kunakotokana na kugonga mwamba juhudi za ujumbe wa Umoja wa Mataifa.”
Abdoulaye Bathily amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York kwamba amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akisisitiza kwamba Umoja wa Mataifa “hauwezi kusonga mbele kwa mafanikio” katika kuunga mkono mchakato wa kisiasa nchini Libya, mbele ya viongozi wanaoweka “maslahi yao binafsi juu ya mahitaji ya nchi.”
Bathily amewatuhumu viongozi wa Libya kwa kukaidi juhudi za kimataifa za kurejesha amani nchini humo, na “kuchelewesha uchaguzi,” na kuonya kwamba Libya imekuwa “uwanja wa ushindani mkali” kati ya wahusika wa kikanda na kimataifa.
Libya imekuwa katika hali ya ukosefu wa amani na mivutano ya kisaisa tangu baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi mwaka 2011.