Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, imemhukumu raia wa Kenya, Samwel Murwa (25) kutumikia kifungo cha miaka 27 jela kwa kosa la kupatikana na mafurushi saba ya kilo 259 za Mirungi.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Jaji Imaculeti Banzi baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi watano na vielelezo saba vya upande wa mashitaka, ambao alisema ulikuwa ni ushahidi mzito na haukuacha mashaka yoyote.
Awali mawakili wa upande wa mashitaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Sabitina Mcharo na Grace Kabu waliieleza mahakama mshitakiwa alikamatwa na mirungi hiyo Agosti 19,2018 katika kijiji cha Mnoa wilaya ya Mwanga.
Siku hiyo ya tukio, mshitakiwa alikamatwa porini akiwa amekalia mfuko wa Sandarusi ukiwa na mirungi na pembeni yake kulikuwa na mifuko mingine sita yote ikiwa imesheni mirungi ambayo huingizwa nchi kutoka Kenya.
Katika utetezi wake ambao mahakama iliukataa, raia huyo wa Kenya alijitetea kuwa siku hiyo alikamatwa na polisi kwa kuingia nchini bila kibali lakini alivyofikishwa katika gari ya polisi ndio akakuta magunia hayo saba ya Mirungi.
Akisoma hukumu yake, Jaji Banzi alisema ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka ulijitosheleza na haukuacha mashaka na kwamba utetezi wake hauna mashiko kwani hakuwadodosa mashahidi juu ya hicho alichojitetea nacho.