Siku moja baada ya kusitisha mkutano wa ngazi ya juu na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un Rais wa Marekani, Donald Trump amesema mkutano huo huenda ukafanyika kama ilivyopangwa awali.
Alhamisi Trump alitangaza kusitisha mkutano huo uliopangwa kufanyika June 12 huko Singapore akitaja kile alichokiita “hasira kubwa na uadui wa wazi” uliooneshwa hivi karibuni katika taarifa iliyotolewa na Korea Kaskazini.
Siku moja baadae, Trump ameonekana akilegeza msimamo. Ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa “mazungumzo yenye faida kubwa” yanaendelea na Korea Kaskazini juu ya kuhuisha mazungumzo hayo”.
“Kama mazungumzo yatafanyika, basi uwezekano ni kuwa yatabaki Singapore kwa siku ile ile iliyopangwa June 12,” ameongeza Trump.