Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amempa siku mbili Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoni Ruvuma, Gaspar Balyomi, awe amepeleka gari katika shule ya Sekondari Tunduru kwa ajili ya kuwahudumia walimu na wanafunzi shuleni hapo.
Ametoa agizo hilo leo Januari 2, 2021, wakati akikagua ukarabati wa shule ya sekondari Tunduru, baada ya mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate, kumueleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya usafiri.
“Mkurungezi Jumatatu lete gari moja hapa likiwa limeandikwa Shule ya Sekondari Tunduru, lije kutoa huduma kwa watoto na walimu wetu, hii shule ina wanafunzi zaidi ya 600 na walimu 28 lazima iwe na usafiri ambao hata mtoto akiugua afikishwe hospitali” Waziri Mkuu.
Kuhusu ukarabati uliofanyika shuleni hapo, Waziri Mkuu, ameridhishwa na ametumia fursa hiyo kumpomgeza mkuu wa shule, Mwalimu Amini Limia, pamoja na kamati ya ujenzi kwa kazi nzuri ya usimamizi waliyoifanya.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi wazingatie sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa shuleni hapo ili waweze kuishi vizuri. “Someni hasa sasa hivi ni wakati wa likizo mpo hapa mnaendelea na masomo hatutarajii mpate daraja la nne wala sifuri, kila mmoja ahakikishe anasoma na kupata daraja litakalomfikisha chuo kikuu”