Mkutano wa kilele wa kundi la mataifa yanayoinukia kwa kasi kiuchumi la BRICS umeanza leo Jumanne nchini Afrika Kusini chini ya kauli mbiu ya “BRICS na Afrika”.
Ajenda kubwa ya mkutano huo wa 15 ni kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya kundi hilo na bara la Afrika na uwezekano wa kupokea wanachama zaidi katika siku zijazo.
Kundi hilo linaloyajumuisha mataifa ya Brazil, Urusi, India, China na mwenyeji Afrika Kusini linatizamwa kuwa mbadala kwa udhibiti mkubwa sekta za uchumi na fedha duniani ulio chini ya mataifa ya magharibi.
Mkutano huo utakaoendelea hadi siku ya Alhamisi mjini Johannesburg, unahudhuriwa na viongozi wote wa kundi hilo isipokuwa rais Vladimir Putin wa Urusi ambaye atashiriki kwa njia ya video.
Putin anayetakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC atawakilishwa na waziri wake wa mambo ya kigeni Sergei Lavrov.
Baada ya majadiliano Jumanne ya leo Agosti 22 kuhusu uhusiano wa kibiashara wa ndani ya BRICS, viongozi wanne wa kundi hilo wanatarajia kukutana kwa faragha.
BRICS kwa sasa inajumuisha nchi tano – Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini – na upanuzi wa kundi hilo unatarajiwa kuwa ajenda kuu katika mkutano huo.
Nchi zingine ambazo zimeomba kujiunga na BRICS ni pamoja Algeria, Argentina, Bangladesh, Bahrain, Belarus, Bolivia, Cuba, Misri, Ethiopia, Honduras, Indonesia, Iran, Kyrgyzstan, Kuwait, Morocco, Nigeria, Palestina, Saudi Arabia, Senegal, Thailand, Muungano wa Falme za Kiarabu, Venezuela na Vietnam.