Mkutano wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa, COP28 umezindua siku ya Alhamisi, mfuko wa kufidia hasara na uharibifu utokanao na mabadiliko ya tabianchi kwa mataifa yalioko hatarini kuhusiana na ongezeko la joto duniani.
Wakati viongozi wa kimataifa wakikusanyika Dubai kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi Duniani, wajumbe wanatarajia kufikia makubaliano ya mapema kuhusu juhudi za kukabiliana na majanga.
Mazungumzo ya wiki mbili yanayofanyika mwaka huu katika jiji hilo la Ghuba lililong’aa yanakuja katika wakati muhimu, huku uzalishaji wa hewa ukaa bado ukiongezeka na mwaka huu unatarajiwa kuwa na viwango vya juu vya joto zaidi katika historia ya binadamu.
Mfalme wa Uingereza Charles III, viongozi wa dunia, wanaharakati na watetezi wa mazingira ni miongoni mwa zaidi ya watu 97,000 wanaotarajiwa kuhudhuria kile kinachotajwa kuwa mkutano mkubwa zaidi wa mabadiliko ya tabia nchi wa aina yake.
“Tumewasilisha historia leo,” rais wa UAE wa COP28,Sultan Al Jaber aliwaambia wajumbe, akiongeza kuwa nchi yake ilikuwa ikitoa dola milioni 100 kwa mfuko huo. Ujerumani pia imeahidi kutoa dola milioni 100.
Baada ya miaka mingi ya kujiburuza juu ya suala hilo, mataifa tajiri yaliunga mkono mfuko huo katika makubaliano ya kihistoria katika mkutano wa kilele wa COP27 mjini Sharm el-Sheikh nchini mwaka jana.