Katibu Mkuu wa Hezbollah Naim Qassem alisema Jumatano kwamba kundi lake liliwasilisha maoni kuhusu pendekezo la Marekani la kusitisha uchokozi wa Israel dhidi ya Lebanon, akibainisha kwamba makubaliano sasa yanategemea jibu la Israel na “uzito” wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Katika hotuba ya televisheni, Qassem aliashiria uthabiti wa Hezbollah kwenye medani ya vita, akisema kundi hilo liko tayari kulisababishia hasara kubwa jeshi la Israel. Pia aliweka wazi kuwa Hezbollah haisitishi shughuli zake huku ikisubiri matokeo ya mazungumzo.
“Tulipokea karatasi ya mazungumzo, tukaipitia kwa kina na kutoa maoni yetu,” Qassem alisema, na kuongeza kuwa Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri pia alikuwa na maoni, ambayo yalilingana na msimamo wa Hezbollah.
“Maoni haya yaliwasilishwa kwa mjumbe wa Marekani Amos Hochstein na kujadiliwa kwa kina.”
Qassem alisisitiza kuwa Hezbollah itajizuia kujadili mahususi ya makubaliano yaliyopendekezwa hadi mazungumzo yaendelee kwa utulivu.
Alisisitiza kwamba mafanikio ya mazungumzo hayo sasa yanategemea mwitikio wa Israel kwa maoni yao.
Qassem alisema kanuni za mazungumzo za Hezbollah zimeegemezwa juu ya matakwa mawili makuu: usitishaji kamili na wa kina wa uhasama na uhifadhi wa uhuru wa Lebanon.
“Tunafanya kazi katika nyanja mbili — oparesheni za kijeshi na mazungumzo — na hatutasimamisha shughuli za kijeshi wakati tukisubiri matokeo ya mazungumzo,” alisema.