Mkuu wa polisi nchini Kenya, Japheth Koome, amejiuzulu huku kukiwa na ukosoaji kuhusu jinsi polisi walivyojibu maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 30.
Katika taarifa, Rais William Ruto alitangaza kukubali kujiuzulu kwa Koome kama Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi na kumteua naibu wake, Douglas Kanja, kukaimu mara moja.
Imejiri siku moja baada ya Ruto kufurusha karibu baraza lake lote la mawaziri, akikubali matakwa ya waandamanaji.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na waangalizi wanaoungwa mkono na serikali, wameshutumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, ikiwa ni pamoja na kufyatua risasi za moto kwenye umati wa watu. Awali Ruto alisema uchunguzi utafanywa kubaini kosa la polisi kwa vifo hivyo.
Maandamano yaliyoongozwa na vijana dhidi ya upandishaji kodi uliopangwa yalianza mwezi uliopita. Baadhi ya waandamanaji walivamia bunge kwa muda kabla ya Ruto kutupilia mbali ushuru huo mpya.