Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani amewataka Wasimamizi wa Vyama vya Ushirika wakiwemo Warajis Wasaidizi wa Mikoa kuchukua hatua stahiki kutokana na madhaifu yaliyobainishwa katika Ripoti ya Jumla ya Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika uliofanywa na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
“Kwa kuwa Ripoti ya COASCO huwasilishwa katika mikoa husika, nawaagiza Warajis Wasaidizi wa mikoa kuchukua hatua stahiki kama ilivyoshauriwa na Wakaguzi, kama kuna viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika wamehusika katika kuhujumu mali za wanaushirka; shirikianeni na Vyombo vya Dola katika maeneo yenu ili kunusuru mali za Wanaushirika,” Dkt. Kamani.
Dkt. Kamani ametoa wito huo mara baada ya Kikao kazi cha Makamishna wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine Tume ilipokea Ripoti ya Jumla ya Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika uliofanywa na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
“Warajis Wasaidizi wa Mikoa ninawapa wiki mbili kuwa wamezichambua taarifa za vyama na kuanza kuchukua hatua. Nataka kupata taarifa ya kila hatua na mimi nitafuatilia ana kwa ana. Hatuwezi kuendelea kuwalea watu wasiotaka kuwajibika kwa dhamana waliyopewa na wanachama, na hakuna jiwe ambalo halitapinduliwa kuhakikisha mali na fedha za wanachama zinalindwa,” Dkt. Kamani.
Vyama vya Ushirika 4,413 vimekaguliwa na COASCO kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Vyama Vikuu (Union), Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Mazao (AMCOS), Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na vinginevyo vimefanyiwa ukaguzi.
Akizungumzia kuhusu uhamasishaji na uanzishwaji wa vyama vya ushirika nchini, Dkt. Kamani amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imesajili jumla ya vyama vya ushirika vya msingi 79 na chama cha Mradi wa pamoja mmoja (1) katika kipindi cha miezi mitatu (3) ya Julai hadi Septemba katika kasi ya ujenzi wa ushirika nchini.
Hivyo, idadi ya vyama vya ushirika imeongezeka na kufikia 11,410. Vyama vipya vilivyoanzishwa vina jumla ya wanachama 5,630.
Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Benki ya Kilimo (TADB) wameamua kufuatilia ujenzi wa bwawa kubwa litakalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji wa ushirika kwenye bonde la Kibaigwa wilayani Kongwa na pia ujenzi wa kiwanda cha vifungashio vya mazao.
“Kwa kuwa tumebaini viwanda 107 vinavyomilikiwa na ushirika vinavyohitaji kuimarishwa, naviagiza vyama hivyo kuainisha viwanda vya kipaumbele ili vitengenezewe mchanganuo kwa minajili ya kupunguza usafirishaji nje mazao ya kilimo yakiwa ghafi na kusaidia kuongeza ajira,” Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika
Tume kwa kushirikiana na Wadau wengine imeendelea kufanya uhamasishaji wa uanzishaji wa vyama vya ushirika katika sekta mbalimbali ikiwemo Wakulima wa matunda ya Parachichi na Ndizi, vikundi vya wakulima wa umwagiliaji na vikundi vinavyojishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Dkt. Kamani amesema kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania imedhamiria kuongeza idadi ya wanachama wa vyama vya ushirika hadi kufikia wanachama 15,000,000 ifikapo mwaka 2021 kutoka wanachama 4,611,804 waliopo hivi sasa.