Watu wasiopungua 37 wamefariki dunia katika mripuko uliotokea katika kiwanda kimoja cha kusafishia mafuta kilichokuwa kinifanya kazi kinyume cha sheria huko kusini mwa Nigeria.
Ripoti kutoka Nigeria zinasema kuwa, mripuko huo uliotokea jana umeharibu pia makumi ya nyumba karibu na kiwanda hicho cha kusafishia mafuta katika eneo la Ibaa katika jimbo la Rivers; ambacho kilikuwa kikifanya kazi kinyume cha sheria.
Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo leo Jumanne na kuongeza kuwa, watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mripuko huo wa na tayari wamefikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Inaarifiwa kuwa, wanawake wawili wajawazito ni miongoni mwa makumi ya watu waliopoteza maisha kwenye mkasa huo uliotokea mapema jana Jumatatu jimboni Rivers.
Nigeria ni miongoni mwa nchi wazalishaji wakubwa wa mafuta barani Afrika. Hata hivyo mapato yake ya mafuta yamekuwa yakipungua siku baada ya siku kutokana na kuongezeka hali ya mchafukoge na ukosefu wa usalama.