Watu wasiopungua 30 wamekufa baada ya kituo cha mafuta kushika moto na kusababisha mlipuko mkubwa katika jimbo la kusini mwa Urusi la Dagestan
Mbali ya idadi hiyo ya vifo, mkasa huo kwenye mji mkuu wa jimbo hilo la kusini mwa Urusi wa Makhachkala umewajeruhi wengine 105 ikiwemo watoto 15.
Wizara ya Huduma za Dharura nchini Urusi imesema moto huo ulizuka majira ya usiku kwenye kituo kimoja cha kutengeneza magari na kisha kusambaa hadi kwenye kituo cha mafuta kilicho jirani na kusababisha mlipuko wa kutisha.
Picha na mikanda ya video vilionesha moto mkubwa ukiwaka na jengo moja la ghorofa likitetekea wakati vikosi vya zima moto vikijaribu kupambana kuuzima.
Kufuatia mkasa huo, rais Vladimir Putin ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga na amewatakia afua ya haraka wote wanapatiwa matibabu.