Zambia inakabiliwa na mlipuko mkubwa wa kipindupindu ambao umeua zaidi ya watu 400 na kuambukiza zaidi ya 10,000, na kusababisha mamlaka kuamuru shule nchini kote zifungwe baada ya likizo za mwisho wa mwaka.
Uwanja mkubwa wa soka katika mji mkuu umebadilishwa kuwa kituo cha matibabu.
Serikali ya Zambia inaanzisha mpango wa chanjo kubwa na inasema inatoa maji safi lita milioni 2.4 kwa siku – kwa jamii ambazo zimeathirika katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Wakala wa Taifa wa Kukabiliana na Maafa umehamasishwa.
Wizara ya Afya inasema ugonjwa wa kipindupindu umegunduliwa katika karibu nusu ya wilaya za nchi hiyo na mikoa tisa kati ya 10, na taifa la takriban watu milioni 20 limekuwa likirekodi zaidi ya kesi 400 kwa siku.
“Mlipuko huu unaendelea kuwa tishio kwa usalama wa afya ya taifa,” Waziri wa Afya Sylvia Masebo alisema, akielezea kuwa ni shida ya nchi nzima.