Mlipuko wa Mpox umeua watu 548 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwanzo wa mwaka huu na sasa unaathiri mikoa yote, Waziri wa Afya Samuel-Roger Kamba ametangaza siku ya Alhamisi, Agosti 15.
Kulingana na ripoti ya hivi punde ya magonjwa ya mlipuko, “nchi DRC imerekodi kesi 15,664 zinazowezekana na vifo 548 tangu mwanzo wa mwaka,” amesema.
Kufikia Agosti 3, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani, Africa CDC kilikuwa kimerekodi vifo 455 na maambukizi 14,479 katika mikoa 25 kati ya 26 ya nchi hiyo.
Kama ukumbusho, Jumatano hii, Shirika la Afya Duniani, WHO, lilianzisha kiwango chake cha juu zaidi cha tahadhari ya kiafya katika kiwango cha kimataifa katika kukabiliana na kuibuka tena kwa visa vya ugonjwa wa Mpox barani Afrika.
“Leo kamati ya dharura ilikutana na kunifahamisha kwamba kwa maoni yao hali hiyo ni dharura ya afya ya umma inayotia wasiwasi katika ngazi ya kimataifa. Nilikubali ushauri huu,” Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema katika mkutano na waandishi wa habari. “Hii ni hali ambayo inapaswa kutuhusu sisi sote,” alisema.
Virusi hivyo vinavyoambukiza binadamu, ni hasa kutoka kwa wanyama mbalimbali wa porini, panya au nyani kwa mfano. Uambukizaji kutoka kwa binadamu hadi kwa binadamu ni mdogo, linaeleza Shirika la Afya Duniani (WHO).
Dalili zake ni sawa, lakini sio mbaya sana, na zile zilizozingatiwa hapo awali kwa watu wanaougua ndui: homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, maumivu ya mgongo, wakati wa siku tano za kwanza. Kisha upele huonekana (kwenye uso, viganja vya mikono, nyayo za miguu), vidonda.
Mpox iligunduliwa kwa mara ya kwanza kwa binadamu mnamo mwaka 1970 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (zamani Zaire) kwa mvulana wa miaka 9 aliyeishi katika eneo ambalo ugonjwa wa Mpox ulikuwa umeangamizwa tangu mwaka 1968. Tangu 1970, kesi za wanadamu za Mpox ziliripotiwa katika Nchi 10 za Kiafrika.