Upande wa Mashtaka umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa inasubiri ripoti ya kielelezo kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kuhusu kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride inayomkabili Shamim Mwasha (41) na mumewe, Abdul Nsembo(45).
Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi, Kelvin Mhina wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Wankyo amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo anaomba ahirisho la kesi hiyo wakati wakisubiri majibu ya kielelezo kutoka kwa Mkemia Mkuu.
Hata upande wa utetezi umeomba kupewa taarifa kuhusu kukamilika kwa ripoti hiyo.
Katika majibu yake Wakili Wankyo ameutaka upande wa utetezi wawe wavumilivu kwa sababu yeye si msemaji wa Ofisi ya Mkemia Mkuu.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 8, 2019. Washtakiwa wamerudishwa rumande.
Washtakiwa hao wanatuhumiwa kusafirisha dawa hizo za kulevya, Mei 1,2019 wakiwa eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam kinyume na sheria ya uhujumu uchumi.
KIBANDA UMIZA KIGOMA ”KOCHA MBINAFS, SAMATTA ANAKUA MPWEKE ANAONEKANA WA KAWAIDA”