Leo Alfajir ya July 5, 2018 Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa DSM, Marison Mwakyoma aliongozana na Kaimu Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya DSM DCP- Lebaratus Sabas wamefanya ukaguzi wa leseni za madereva na ubovu wa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani.
Akizungumzia zoezi hilo, DCP- Lebaratus Sabas ambaye pia ni Mkuu wa Operation ya Polisi Tanzania amesema zoezi hilo lililoanza majira ya saa 11 Alfajiri ni endelevu na linafanyika kuhakikisha Jeshi la Polisi linakabiliana na wimbi la ajali.
“Wapo waliokutwa wana leseni feki, yapo magari ambayo yamekutwa hayana ubora wa kusafirisha abiria na zoezi linaendelea nchi nzima, ninavyozungumza hivi popote walipo madereva na magari yao wajue kabisa kwamba zoezi hili watakutana nalo iwe Mwanza, iwe Kigoma, iwe Mtwara, iwe Lindi, iwe Ruvuma” amesema Liberatus Sabas
Naye RTO wa DSM, Marison Mwakyoma amesema kuwa zoezi hilo limekuja baada ya kugundua kuwa baadhi madereva wana leseni feki pamoja na ukosefu wa elimu kwa madereva ambapo wengi wao wanaogopa Trafiki badala ya kuogopa sheria.
“Tunataka watu waogope sheria wasiogope trafiki asilimia kubwa ya madereva wanaogopa trafiki na ndio maana akifika njiani anakuuliza mwenzake ‘huko vipi?’ akishamwambia kupo salama anapita anaendesha mwendo,” amesema Mwakyoma