Mbivu na mbichi kuhusu Ubunge wa Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu itajulikana katika Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo inasikiliza maombi ya kesi yake namba 18/2019.
Hatua hiyo ya kusikilizwa inatokana na pingamizi za Upande wa Serikali kupinga Mahakama hiyo kusikiliza maombi hayo kutupiliwa mbali.
Maombi ya Lissu kutetea ubunge wake wa Singida Mashariki yanasikilizwa mahakamani hapo mbele ya Jaji Sirilius Matupa.
Lissu amefungua maombi Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dar es Salaam chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.
Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungau shauri la maombi maalum kwa lengo la kupata amri mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge.