Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwafunguliwa mashtaka wanaosambaza taarifa za uongo na za kutengeneza kuhusu matukio ya utekaji na kupotea watu ambayo yanachafua taswira ya Serikali.
Waziri Lugola amesema, watu hao wanakaa mitandaoni asubuhi hadi jioni wakizusha matukio hayo machafu wakiwa na lengo la kupata umaarufu wa kisiasa kuichafua Serikali ya Rais John Magufuli na wananchi wake ambayo inafanya kazi nzuri kuiletea nchi maendeleo kwa kasi zaidi.
Lugola ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara alipokuwa anajibu maswali mbalimbali ya wananchi wa Mji Mdogo wa Kisorya, Kata ya Kisorya, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo, ambapo mara baada ya kuruhusu maswali, mmoja wa wananchi hao alimuuliza Waziri huyo kuhusu Wizara yake imejipangaje kuyasambaratisha matukio ya utekaji, pamoja na kupotea watu ikiwemo tukio la kupotea kwa Mwandishi wa Habari ambalo linaendelewa kujadiliwa katika mitandao ya kijamii nchini.