Serikali imefuta miliki ya Mashamba matatu ya Mkomazi Plantantions maarufu MOA yaliyopo wilaya ya Mkinga mkoani Tanga kutokana na kukiuka masharti ya uendelezaji ikiwemo kutelekezwa bila kufanyiwa maendelezo yaliyokusudiwa na kutolipiwa kodi ya pango la ardhi.
Uamuzi huo umetangazwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alipozungumza na wananchi wa Mayomboni wilayani Mkinga alipokwenda kutatua mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo.
Mashamba yaliyofutiwa hati yote matatu yana ukubwa wa ekari 15,738.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema uamuzi wa kufuta mashamba hayo matatu unafuatia maombi yaliyotumwa kwa Raisi John Pombe Magufuli ya kutaka kufutwa mashamba hayo kutokana na kutoendelezwa na wamiliki wake kwa muda mrefu.Rais ameridhia maombi hayo kwa kuwa serikali imekuwa ikisisitiza utekelezwaji wa sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999 ikiwemo uendelezaji wa mashamba ambayo yamemilikishwa sehemu mbalimbali nchini.