Mwanaume mmoja wa Nigeria aitwae Chukwuebuka Kasi Obiaku mwenye umri wa miaka 34 amekamatwa na Polisi wa Nigeria kwa kosa la kumteka Mwanamke mzungu Raia wa Marekani mwenye umri wa 64 baada wawili hao kukutana na kuanzisha mapenzi kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.
Unaambiwa Obiaku alimshawishi Mwanamke huyo kusafiri kutoka Washington DC mpaka Nigeria February mwaka 2019 na wakafunga ndoa miezi mitatu baada ya kuwasili Nigeria ambapo Polisi wanasema hiyo ya kufunga ndoa ilikua ni kama zuga tu ili Bibi aone kapendwa kwelikweli ila jamaa alikua anaplan zake kitambo ambapo alifanikiwa kumlaghai USD 48000 ambazo ni zaidi ya Tsh. milioni kumi na moja.
Kilichotokea muda mfupi baada ya ndoa ni kitumbua kuingia mchanga, Jamaa alimgeuza Bibi huyo kuwa mateka, alimuamrisha kuwa chini ya amri ya kutofanya chochote kinyume na maagizo na alimshikilia mateka hotelini kwa zaidi ya mwaka mmoja na akawa anamuamrisha kuomba pesa kwa Watu na Makampuni mbalimbali.
Mnigeria huyo alimlazimisha Bibi huyo wa miaka 64 kutumia lafudhi yake ya kimarekani kuomba Watu pesa pamoja na Taasisi mbalimbali ambapo pamoja na hayo Jamaa alichukua kwa lazima kadi za Benki za Bibi huyo na akawa kila mwezi anachukua pesa za mafao alizokua akitumiwa Bibi huyo ambaye ni Mstaafu wa Serikali ya Marekani ambapo kila mwezi kwa miezi 15 Obiaku alikua akichukua pesa.
Obiaku bado anaendelea kushikiliwa na anaweza kushitakiwa kwa makosa ya mitandao ambapo Polisi wanasema wakati anahojiwa amekiri kwamba alifunga ndoa na huyo Bibi ili kumuaminisha kuwa kapendwa, sasa ilikuaje mpaka ikagundulika kwamba Jamaa kamteka Bibi na kumshikilia Hotelini? Polisi wanasema kuna Msamaria ambaye pia ni Mnigeria ndiye aliewatonya.
Polisi wa Nigeria wamesema kuna kesi nyingine kama hii ya Mwanaume Mnigeria kumteka Mwanamke Mfilipino mwenye umri wa miaka 40 ambao nao pia walikutana na kuanzisha mapenzi kupitia facebook, alipokwenda Nigeria akamteka kwa miezi 6 na kumzuia kurudi Ufilipino.