January 15, 2019 Rais Dkt. John Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Bharti Airtel ya India juu ya umiliki wa hisa za Kampuni Airtel Tanzania na maslahi mengine ya Tanzania kutokana na biashara ya kampuni hiyo.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika Ikulu Jijini DSM ambapo Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi ametia saini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mwenyekiti wa Bharti Airtel Sunil Mittal ametia saini kwa niaba ya Kampuni ya Bharti Aitel.
Prof. Kabudi amesema katika makubaliano hayo kampuni ya Bharti Airtel imekubali kupunguza umiliki wa hisa zake za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 60 hadi 51 na hivyo kuongeza hisa za Serikali kutoka asilimia 40 hadi 49 bila malipo yoyote kutoka Serikalini.
Prof. Kabudi “Serikali kupata gawio la kila mwaka kutokana na umiliki wake wa asilimia 49 ambapo inakadiriwa itakuwa ikipata Bilioni 10, kufutwa kwa madeni yote ya kampuni ya Airtel yaliyokuwa yamefikia Trilioni 1, Bharti Airtel itatoa Bilioni 1 kila mwezi kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia Aprili 2019 ili kuonesha nia njema na Bharti Airtel itatoa Bilioni 2.3 kwa ajili ya kuchangia huduma za kijamii.
Kwa upande wake Sunil Mittal amesema amefurahishwa na kufikiwa kwa makubaliano katika mazungumzo hayo na amebainisha kuwa awali aliona kuna ugumu wa kufikia makubaliano lakini baadaye alielewa kuwa lengo la Rais Magufuli ni kuhakikisha anaweka mwelekeo mzuri wenye manufaa kwa Tanzania.
Rais Magufuli ameipongeza timu iliyoiwakilisha Serikali ya Tanzania chini ya Prof. Kabudi na timu ya Mittal kwa kufikia makubaliano hayo yaliyochukua muda wa miezi 8 na ameelezea furaha yake kuwa sasa Airtel Tanzania itaanza kutoa manufaa kwa Serikali ikiwemo gawio na maslahi mengine yanayostahili, mambo ambayo hayakufanyika kwa miaka zaidi ya 8 tangu kampuni hiyo ianzishwe hapa nchini.
JPM amempongeza Mittal kwa kuridhia kuongeza hisa za Serikali, kutoa Bilioni 1 kila mwezi kwa miaka 5 na kutoa mchango wa Bilioni 2.3 ambazo ameagiza ziungane na Bilioni 1 iliyotengwa kwa ajili ya sherehe za siku ya Uhuru za mwaka 2018 (na kufanya jumla shilingi Bilioni 3.3) kwenda kujenga hospitali katika makao makuu ya nchi Jijini Dodoma.
“Huu ndio uwekezaji ninaoutaka, uwekezaji ambao tuna faida nao, Airtel ilikuwepo tangu miaka 8, 9 iliyopita lakini tulikuwa hatupati kitu, sasa tutapata fedha, na hili liwe somo kwetu Watanzania wote kuwa Serikali inapotetea maslahi ya Watanzania haizungumzi kutoka hewani, tujifunze kuwaheshimu watalaamu wetu” amesisitiza Rais Magufuli.
RAIS MAGUFULI AAMUA ZAIDI YA BILIONI 3 ZIKAJENGE HOSPITALI YA DODOMA