Taarifa zinasema kuwa nyota wa Liverpool Mohamed Salah ataondoka klabuni hapo baada ya kucheza mechi yake ya mwisho dhidi ya Newcastle.
Mo Salah amekuwa akihusishwa na kutaka kuondoka Liverpool wiki za hivi karibuni huku Al-Ittihad wakitangaza kumtaka Mmisri huyo.
Msimu huu wa kiangazi, Liverpool tayari imeuza wachezaji wawili kwenye Ligi Kuu ya Saudia. Wote wawili Jordan Henderson na Fabinho waliruhusiwa kuondoka Merseyside kwa kiasi kikubwa cha pesa.
Kwa hali ilivyo sasa wanakaribia kupoteza mchezaji mwingine nyota, huku ripoti zikisema kwamba Mmisri huyo ataondoka kwa ajili ya matibabu na kukamilisha uhamisho wa kwenda Al-Ittihad.
Kwa mujibu wa Riyadiyatv, mtangazaji wa michezo nchini Saudi Arabia, Salah atakamilisha uhamisho wa kwenda Al-Ittihad na kuondoka Anfield kabla ya dirisha la uhamisho kufungwa.
Inaripotiwa kuwa Salah amecheza mechi yake ya mwisho akiwa na Liverpool dhidi ya Newcastle na atasafiri kuelekea Dubai kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.
Al-Ittihad walitangaza nia yao kwa Salah wiki iliyopita na makubaliano sasa yanaonekana kukaribia kukamilika.
Kulingana na Sport Italia kama ilivyoripotiwa na Express.co, Salah alikuwa amewaarifu Liverpool kwamba angependa kuhamia Saudi Pro League.
Al-Ittihad wanadaiwa kuweka mezani ofa ya zaidi ya pauni milioni 79 kwa ajili ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31.
Kulingana na ripoti hizo, Al-Ittihad iliweka makataa ya Jumatatu ili kubaini iwapo makubaliano ya Salah yanawezekana. Uwezekano kwamba watafanikiwa katika harakati zao unaongezeka.
Baada ya kuwasili kutoka Roma mwaka 2017, mshambuliaji huyo amecheza mechi 307 na kuifungia timu hiyo mabao 187.
Salah amekuwa muhimu kwa mafanikio ya Jurgen Klopp, ambayo ni pamoja na kushinda Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa.