Mshambulizi wa Liverpool Mohamed Salah anasema “amesikitishwa” na klabu hiyo kushindwa kumpa kandarasi mpya – na anaonekana uwezekano mkubwa wa kuondoka kuliko kubaki.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, mfungaji bora wa Liverpool msimu huu akiwa na mabao 12 katika michuano yote, mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Salah alifunga mabao mawili katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Southampton siku ya Jumapili, likiwemo la ushindi kwa mkwaju wa penalti, na kufikisha Liverpool kwa pointi nane kileleni mwa Premier League.
Fowadi huyo wa Misri, ambaye alijiunga na The Reds kutoka Roma mwaka 2017, aliwaambia waandishi wa habari, waliokuwa nje baada ya ushindi huo wa St Mary’s: “Tunakaribia Desemba na sijapokea ofa zozote za kusalia katika klabu hiyo.
“Labda niko nje zaidi kuliko ndani.”
Alipoulizwa kama alikatishwa tamaa kwamba bado hajapokea ofa, Salah alisema: “Bila shaka, ndio.
“Sitastaafu hivi karibuni kwa hivyo nacheza tu, nikizingatia msimu na ninajaribu kushinda Ligi Kuu na ninatumai Ligi ya Mabingwa pia. Nimesikitishwa lakini tutaona.”
Liverpool hawajazungumza hadharani kuhusu matamshi ya Salah.