Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inatarajia kuendesha kambi ya uchunguzi kwa watoto wenye matatizo ya Mifupa na Kibiongo bure utakaofanyika hopsitalini hapo siku ya tarehe 1/ 05/2024 ikiwa ni sehemu ya kusherehekea siku ya Wafanyakazi Duniani.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Mifupa wa Taasisi ya MOI Dkt. Anthony Assey amesema kambi hiyo ya uchunguzi itagharamiwa na Taasisi ya MOI hivyo ni jukumu la wazazi wenye watoto wenye matatizo ya Mifupa na Kibiongo kuwaleta hospitalini hapo kwa uchunguzi.
“Kwa niaba ya taasisi yetu ya Mifupa Muhimbili MOI, nichukue fursa hii kuwakaribisha wananchi wote wa Dar es Salaam na wa mikoa ya jirani kwa wale wenye uwezo kufika hapa hospitalini MOI siku hiyo ya tarehe 1/05/2024 saa mbili asubuhi kufanyiwa uchunguzi kwa watoto wenye matatizo ya mifupa pamoja na viungo” amesema Dkt. Assey na kuongeza kuwa
“Gharama za uchunguzi huu zitachukuliwa na taasisi, wananchi wote wanakaruibisha …huu utakuwa mwanzo wa kufanya hivyo kwa watu wazima wenye matatizo ya mgongo na mifupa kuwa laini kwa akina mama kwa siku zijazo…tunatarajia kuwahudumia watoto 200 kwa siku ya Mei Mosi”
Meneja Upasuaji wa Mifupa Idara ya watoto Daktari bingwa mbobezi Dkt. Bryson Mshana amesema uwamzi huo umelenga kusogeza huduma kwa jamii na kwamba watoto wenye matatizo ya matege, mguu kifundo, mgongo kupinda, majeraha yaliyotibiwa na kuacha ulemavu, majeraha yasiyotibiwa na watoto wenye shida ya nyonga waletwe hospitalini hapo kwa uchunguzi.
Dkt. Emanuel Lema wa Taasisi ya MOI amesema matatizo ya ulemavu kwa watoto yanaweza kuepukika kwa wanawake kupata lishe bora ikiwemo madini ya folic acid miezi mitatu kabla ya ujauzito ili kuepuka kujifungua watoto wenye ulemavu wa mguu kifundo vichwa vikubwa na mdongo wazi.