Shirika la Anga la Japan (JAXA) limekumbwa na tukio la Moto mkubwa uliozuka Jumanne Novemba 26 katika Kituo chake cha majaribio ya Roketi kilichopo Tanegashima, Mkoani Kagoshima ambapo Moto huo ulianza wakati wa jaribio la Injini ya Roketi aina ya Epsilon S na hata hivyo hakuna Majeruhi waliyoripotiwa kufikia sasa na uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.
Kulingana na JAXA jaribio lilianza saa 2:30 asubuhi kwa saa za Japan na baada ya sekunde 30 mlipuko mkubwa ulitokea ambapo katika Video ya tukio hilo ilionyesha Moshi mweupe na miale ya Moto vikiongezeka kutoka kwenye eneo la majaribio huku Vipande kutoka kwenye Roketi hiyo vilivyochomoka na kurushwa Baharini kutokana na mlipuko huo.
Ripoti za awali zinaeleza kuwa Moto ulizuka kwenye Injini ya Roketi iliyokuwa kwenye jukwaa la usawa wa kuruka ambapo miale ya Moto ilionekana mara tu baada ya jaribio kuanza na Vyombo vya habari vilikuwa umbali wa takribani mita 600 kutoka eneo la tukio lakini hakuna athari zilizoripotiwa upande huo.
Hii si mara ya kwanza JAXA kukutana na changamoto katika programu zake za Roketi ambapo mwezi Februari mwaka huu shirika hilo lilizindua kwa mafanikio Roketi yake mpya ya H3 ambayo imekuwa ikilinganishwa na Falcon 9 ya SpaceX, hata hivyo Moto wa sasa ni pigo lingine kwa juhudi za maendeleo ya Teknolojia ya anga ya Japan.
Juhudi za kuzima Moto na uchunguzi wa kiufundi zinaendelea huku JAXA ikiahidi kutoa taarifa zaidi pindi chanzo cha tukio hilo kitakapobainika na Shirika hilo lina matumaini ya kurejea haraka katika harakati zake za utafiti na uvumbuzi.