Wakati Jose Mourinho akiendelea kulalamika kuwa waamuzi wa ligi ya England wanaionea timu yake, kocha huyu anapaswa kujilaumu mwenyewe kwa kushindwa kuwa mbele ya wapinzani wake wa karibu Manchester City kwa pointi saba mpaka sasa.
Hii ni kwa sababu kiungo Frank Lampard aliruhusiwa kuondoka kwenye klabu hii ya London na kujiunga na timu ya ligi ya Marekani, New York City FC kabla ya kujiunga na Manchester City kwa mkopo mpaka mwisho wa msimu.
Katika muda wake akiwa anaichezea City, Lampard ameweza kuisaidia timu hii kushinda pointi saba kutokana na kiwango alichoonyesha mabapo amechangia timu hiyo kutoka sare na kushinda mechi nyingine mbili kutokana na magoli yake.
Lampard ameifungia City mabao muhimu ambayo yameifanya timu hiyo kuifikia Chelsea na kufanya timu hizo zilingane kwa pointi katika mbio za ubingwa wa England.
Bao lake la kwanza muhimu alifunga kwenye mechi dhidi ya Chelsea ambako alinyanyuka toka benchi na kuisawazishia timu yake iliyokuwa inaelekea kufungwa 1-0 dhidi ya timu yake ya zamani.
Bao hilo kwenye dakika ya 85 sio tu liliipa City pointi moja muhimu bali liliwapokonya Chelsea pointi mbili huku akifunga mabao ya ushindi kwenye mechi dhidi ya Leicester City ambako alifunga mabao mawili na kwenye mechi dhidi ya Sunderland.
Timu hizi zimelingana lakini Chelsea wangeweza kuwa mbele endapo wangekuwa na Lampard ambaye ameonyesha kuwa na mchango mkubwa sana kwa timu yake msimu huu na kama City itatwaa ubingwa basi mchango wa Lampard kwenye ubingwa huo utakuwa mkubwa sana.