Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameigiza Wizara ya Nishati kuhakikisha ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme wa Gridi ya Taifa cha Inyonga kukamilika ifikapo Oktoba mwaka 2023 na mkoa wa Katavi unaunganishwa katikaGridi ya Taifa.
Makamu wa Rais amesema alipokuwa akizungumza na viongozi na wananchi wa Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi katika eneo la Inyonga Wilaya ya Mlele.
Makamu wa Rais ameonesha kutoridhishwa na
kasi ya ujenzi wa mradi huo ambao umechelewa kwa takribani miezi nane mpaka sasa.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka wakurugenzi kuacha mara moja tabia ya kutoza ushuru kwa mazao yanayosafirishwa chini ya tani
moja kwani serikali ilionmdoa tozo hizo ili kuwasaidia wakulima wadogo kupata kipato.
Amesema wakurugenzi wanapaswa kutafuta mbinu sahihi za kuwabaini wanaokusanya mazao zaidi ya tani moja ili kuwanusuru wale wakulima wadogo.
Pia Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa Mlele kuendelea kutafuta elimu kuhusu lishe ili wananchi wa mkoa huo wawe na afya bora kulingana na mazao mengi wanayozalisha.
Makamu wa Rais amewataka kuendelea na juhudi za kutunza mazingira ikiwemo kupiga vita uchomaji
miti na uchafuzi wa mazingira.