Baada ya rais wa Bangladesh Mohammed Shahabuddin kulivunja bunge, Ofisi yake imetangaza kuwa imemuachia huru aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa chama cha upinzani cha BNP, Begum Khaleda Zia
Hatua hiyo ni mfululizo wa matukio yanayoendelea baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kujiuzulu na kukimbilia uhamishoni kutokana na maandamano yaliyodumu kwa karibu mwezi mmoja katika taifa hilo la Asia.
Begum Khaleda Zia, mwenyekiti wa Chama cha BNP ambaye amekuwa mpinzani mkuu wa Sheikh Hasina kwa miongo kadhaa, amewekwa huru kutoka katika kifungo cha nyumbani alichokuwa akikitumikia.
Awali, Zia alihukumiwa kutumikia kifungo hicho jela kwa makosa ya rushwa mnamo mwaka 2018. Alianza kutumikia kifungo cha nje kutokana na sababu za kiutu mwaka 2022 baada ya serikali kusitisha kifungo chake gerezani.
Taarifa ya ofisi ya rais kuhusu kuachiliwa kwake imesema pia kuwa mchakato wa kuwaachilia wafungwa wengine wa kisiasa wakiwemo watu waliokamatwa wakati wa vuguvugu la wanafunzi la kupinga ubaguzi katika mgawanyo wa nafasi za kazi tayari umeanza.
Hayo yanajiri muda mfupi baada ya Rais Mohammed Shahabuddin kulivunja bunge. Kulingana na taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisi ya Rais uamuzi wa kulivunja bunge umefikiwa baada majadiliano na wakuu wa utumishi wa jeshi, viongozi wa vyama vya siasa, wawakilishi wa asasi za kiraia na viongozi wa wanafunzi walioanzisha maandamano.