Mradi wa mpango wa uwekezaji wa huduma ya Mama na mtoto (TMCHIP) umelenga kuboresha afya ya Mama na mtoto pamoja na wananchi wote kwa kuboresha miundombinu yakiwemo majengo, ajira, uboreshaji wa huduma za rufaa na kununua vifaa na vifaa tiba ili kuwa na huduma za uhakika hususan za kundi hilo hapa nchini.
Hayo yamebainishwa Disemba 12, Mwaka huu na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Grace Magembe wakati akifungua mafunzo ya utekelezaji wa mradi wa TMCHIP katika ukumbi wa hoteli ya Cherry iliopo Mkoani Morogoro yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo na kuongeza uelewa wa watendaji na wataalam wa sekta ya afya.
Akifafanua zaidi Naibu katibu huyo, amesema mradi huo unaogharimu zaidi ya Tsh. Bil 16 unalenga kupunguza vifo vya Mama na mtoto ambapo hadi sasa imepunguza kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mpaka 104 kwa kila vizazi hai 100,000 ikiwa ni zaidi ya 80%, hivyo mradi huo una malengo mahsusi ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
“…Mradi huu ambao tunaongelea hapa ni mradi ambao umejikita kuboresha afya ya Mama na mtoto lakini sio afya ya Mama na mtoto pekee bali na afya ya wanannchi wote…” amesema Dkt. Grace Magembe
Aidha, Dkt. Grace amesema mradi huo umepanga kutoa ajira kwa watumishi 1000 ambapo mpaka sasa mradi huo wameajiriwa watumishi 700 na ajira 300 kutangazwa hivi karibuni.
Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amewataka wataalam na wasimamizi hao kusimamia vema miundombinu inayojengwa na mradi huo kwa kutekeleza kwa ufanisi na kuzingatia thamani ya fedha kuendana na ubora wa mradi (Value for money) ili kuwa na miundombinu bora itakayotumika kizazi cha sasa na kijacho.
Sambamba na hayo Dkt. Magembe amewasisitiza kuwa, katika kutekeleza miradi hiyo waepuke uharibifu wa mazingira ili kumuunga Mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupiga vita uharibifu wa mazingira huku akiwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha maeneo yanayopendekezwa kutekeleza miradi husika yawena hati ili kuepuka migogoro baada ya mradi kuanza kutekelezwa.