Baada ya kufanikiwa kupiga ‘hat-trick’ (mabao matatu) ya pili mfululizo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Komorozine ya Comoro, mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa, amebakiza bao moja kumfikia aliyekuwa mfungaji bora wa mashindano hayo msimu uliopita.
Alexis Youngouda Kada wa timu ya Coton Sport ya Cameroon, ndiye aliyeibuka mfungaji bora katika michuano hiyo msimu uliopita kwa kuzifumania nyavu mara saba.
Mpaka sasa Ngassa ameshazifumania nyavu mara sita katika mashindano hayo baada ya kushuka dimbani mara mbili, hivyo amebakiza bao moja afikie rekodi ya Alexis.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam ambao Yanga ilishinda mabao 7-0, mchezaji huyo alizifumania nyavu mara tatu.
Alifanya hivyo tena juzi Jumamosi ambapo timu hiyo ilipambana na Komorozine katika mechi ya marudiano iliyofanyika nchini Comoro ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-2, matatu kati ya hayo yakifungwa na Ngassa
Habari hii kwa hisani ya www.salehjembe.com