BOHARI ya Dawa (MSD) imesema bidhaa za afya, hususani dawa zina utaratibu maalumu wa utunzaji na matumizi yake, ambapo dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi haziruhusiwi kusambazwa, wala kutumika ndani ya bohari.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na MSD na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano MSD Etty Kusiluka ilisema bohari imesikitishwa na taarifa iliyotolewa juzi February 18, 2023 Gazeti la Nipashe toleo Na. 0581225 yenye kichwa cha habari “Wagonjwa wapewa dawa zilizoisha muda wa matumizi” katika ukurasa wake wa kwanza na wa pili.
“Bohari ya Dawa (MSD) imesikitishwa na taarifa iliyoripotiwa na gazeti hilo ambapo kichwa cha habari cha taarifa hiyo na kile kilichoripotiwa ndani ya taarifa husika haviendani hivyo kusababisha taharuki kwa wananchi, vituo vya kutolea huduma za afya nchini, Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla”
Alisema uongozi wa MSD umesikitishwa na upotoshaji huo ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 36 kifungu kidogo cha (1-3) cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016;taarifa hiyo, imeharibu taswira ya MSD na hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 50 (1) (a) (i) na (ii) cha Sheria ya Habari, kitendo hicho ni kosa la jinai.
“Kutokana na hilo, MSD, inalitaka gazeti la Nipashe kukanusha taarifa hii na kuomba radhi kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti lake, kama ilivyoripotiwa tarifa hii tarehe 18 Februari, 2023 kwa siku tatu mfululizo,”alisema.
Aliongeza kuwa “Tungependa umma utambue kwamba bidhaa za afya, hususani dawa zina utaratibu maalumu wa utunzaji na matumizi yake, ambapo dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi haziruhusiwi kusambazwa, wala kutumika. MSD inafuata utaratibu wa usimamizi wa bidhaa za afya ambao upo kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Dawa na Vifaa Tiba Na. 219 ya mwaka 2021 na Sheria ya Utunzaji wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004, chini ya Wizara ya Afya,”alisema.
Alisisitiza kuwa MSD ina utaratibu wa ndani unaozuia dawa zilizobakiza miezi mitatu kuisha muda wa matumizi (expiry) kutoka katika maghala yake kote nchini.
Dawa zinazoisha muda wake wa matumizi katika maghala ya MSD hutengwa kwenye sehemu maalumu zikisubiri hatua za uteketezaji kwa kufuata taratibu na sheria zinazosimamia uteketezaji wa dawa.
Aidha, ieleweke kuwa, MSD inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya na si Mwananchi mmoja mmoja (mgonjwa), na hivyo kuondoa uwezekano wa dawa zilizoisha muda wake kumfikia mgonjwa kama ilivyoripotiwa kwenye kichwa cha habari cha taarifa hiyo.
Etty alisema MSD itaendelea kuwa na mawasiliano na MSD badala ya kuandika taarifa za upande mmoja.
“ MSD iko tayari kutoa ushirikiano kwa mwandishi yeyote anayehitaji taarifa za majukumu ya MSD, ama ufafanuzi wa suala lolote kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazosimamia utoaji habari,”alisema.