Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, amesema Idara hiyo imeandaa programu maalum ya taarifa ya maendeleo ya miradi Mikoani ambayo itazinduliwa Jijini Dodoma Jumatano Nov 01,2023, itakayowapa nafasi Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zao kuwaeleza Wananchi wao ni nini Serikali imefanya katika Mkoa.
Akiongea na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam leo, amesema “Idara ya Habari (MAELEZO) imeandaa programu maalum ya taarifa ya maendeleo ya miradi Mikoani, na programu hii tunakwenda kuizindua Jumatano November 01,2023 Mkoani Dodoma, November 02 tutakuwa Morogoro, November 03 Pwani na November 04 Dar es salaam, ni programu itakayowapa nafasi Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zao kuwaeleza Wananchi wao ni nini Serikali imefanya katika Mkoa”
“Kwahiyo tutafika katika Mkoa tutamwita Mkuu wa Mkoa atakuja na Wakuu wake wa Wilaya lakini tunataka tuwape nafasi Wakurugenzi kwasababu tunataka kusikia habari za utekelezaji”
“Katika muundo wetu fedha zinapelekwa kwenye Halmashauri kule ndio utekelezaji unakwenda ukisikia Shule, Hospitali imejengwa ni Afisa Elimu, Mtu wa Afya, Mhandisi, Boss wao nani? Mkurugenzi hii ndio sababu tumewachagua Wakurugenzi, sio kama tumemruka Kiongozi mwingine, tunataka Watanzania wajue Serikali inafanya nini kwenye Halmashauri, Serikali inafanya mambo mengi ila Wananchi hawana habari”